Jumamosi 21 Novemba 2026 - 23:10
Mashia Hawajawahi Kuingia Katika Vita Visivyo na Manufaa, na Wamelipa Gharama Kubwa Katika Kuilinda Lebanon

Hawza/ Naibu Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Kiislamu la Mashia nchini Lebanon amekosoa vikali viongozi wa Lebanon kwa kusalimu amri mbele ya masharti na maagizo ya Marekani pamoja na madola ya kigeni, huku akitaka sera za kitaifa zipitiwe upya.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sheikh Ali al-Khatib, Naibu Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Kiislamu la Mashia nchini Lebanon, katika khutuba ya Swala ya Ijumaa iliyotolewa katika makao makuu ya baraza hilo, amewataka viongozi wa Lebanon kuyachunguza kwa makini mabadiliko ya kikanda na kimataifa, kuacha matumaini yasiyo na msingi yanayoweza kuiletea nchi hasara, na kujiepusha na kukubali maagizo ya Marekani na madola ya kigeni. Pia amewataka kuacha kutoa mawaidha kwa Mashia wa Lebanon, ambao wamelipa gharama kubwa katika kuilinda nchi yao na kila sehemu ya ardhi yake.

Hakuna uhuru wa kweli chini ya uvamizi, utegemezi na maagizo ya kigeni

Akizungumzia maadhimisho ya miaka 83 ya Uhuru wa Lebanon, Sheikh al-Khatib alisisitiza kuwa hakuna uhuru wa kweli katika mazingira ya uvamizi, utegemezi, utawala wa mabavu na kusalimu amri mbele ya maagizo ya kigeni. Aidha, alisifu msimamo wa Kamanda wa Jeshi la Lebanon, Jenerali Haikal, kuhusu suala hilo.

Alisema: “Leo tunakaribia kuadhimisha miaka 83 ya Uhuru wa Lebanon. Hiki ni kipindi muhimu kwa taifa, kinachoturudishia maswali makubwa kuhusu maana halisi ya mamlaka ya kitaifa, uhuru na heshima katika nchi ambayo bado inakabiliwa na changamoto tata za kiusalama, kisiasa na hata zinazohusu uwepo wake wenyewe.

Uhuru, katika maana yake halisi, si tarehe inayotajwa katika hotuba wala siku ya mapumziko kwenye kalenda. Bali ni dhamira ya kweli ya kujikomboa kutoka katika aina zote za utegemezi, kunyenyekea na kutawaliwa na mataifa ya kigeni, pamoja na kujifunga kwa dhati katika kuilinda ardhi, wananchi na uhuru wa maamuzi ya kitaifa.

Kwa miongo kadhaa, wananchi wa Lebanon wamelipa gharama kubwa ili kuimarisha uhuru huu na kuilinda mipaka pamoja na mamlaka ya nchi yao dhidi ya tamaa za kigeni na mashambulizi ya mara kwa mara. Muqawama umekuwa daima mstari wa mbele katika kuilinda nchi na kila sehemu ya ardhi yake.

Kuadhimisha upya kumbukumbu ya Uhuru katika kipindi hiki kunatulazimu kuchunguza uelewa na uwajibikaji mabadiliko ya haraka yanayotokea katika ngazi za kikanda, kimataifa na ndani ya nchi. Hii ni kwa sababu kuna shinikizo la kisiasa, kiuchumi na kiusalama linalolenga waziwazi kuisukuma Lebanon katika kukubali mipango na makubaliano yasiyoendana na maslahi ya taifa wala kujitolea wananchi wake.”

Sheikh al-Khatib aliwataka viongozi wa Lebanon kuacha matumaini yasiyo na msingi na kushindwa, pamoja na kusalimu amri mbele ya maagizo ya Marekani na madola ya kigeni, ambayo yanaifanya Lebanon ijikute katika misimamo isiyo na manufaa kwa nchi wala wananchi wake.

Vilevile, aliwataka viongozi hao kuacha kutoa mafunzo na nasaha kwa Mashia wa Lebanon, ambao wamelipa gharama kubwa sana katika kuilinda Lebanon, kuikomboa ardhi yake na kuhifadhi heshima ya wananchi wake.

Kwa mujibu wa kauli zilizotajwa kutoka kwa Marji' Mkuu wa Mashia, Mashia hawajawahi kuingia katika vita visivyo na manufaa, na madai yanayopingana na ukweli huo si sahihi.

Aliongeza kuwa; viongozi wanapaswa kuchambua kwa makini mabadiliko ya kimataifa na kikanda, kuanzia matokeo ya uchaguzi wa Marekani na Israel, hadi msimamo thabiti wa Iran na mhimili wa Muqawama, pamoja na maendeleo ya vita nchini Yemen.

Naibu Mwenyekiti huyo wa Baraza Kuu la Kiislamu la Mashia aliendelea kusema: “Tulishuhudia mkutano wa kwanza wa kihistoria wa aina yake, ulioyakutanisha madola matatu makubwa duniani nchini China. Tunaamini kuwa kama Marekani ingekuwa imefanikiwa kufikia malengo yake iliyojiwekea mwanzoni mwa vita dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, mkutano huo usingefanyika na Wamarekani wasingeshiriki.

Inasikitisha kuona viongozi wa Lebanon wakichukua misimamo mikali dhidi ya sehemu ya wananchi wao, wakati washirika wao wa nje wakitafuta njia inayofaa ya kujiondoa katika vita hivi vya uchokozi.”

Sheikh al-Khatib alisisitiza: “Haikubaliki tena kwa viongozi wa Lebanon kuendelea kufuata sera ya kusubiri na kutegemea mabadiliko ya nje, au kuweka matumaini yao katika ushindi wa kundi moja la kimataifa au kikanda dhidi ya kundi jingine. Haya yanatokea katika kipindi ambacho dunia inapitia mabadiliko nyeti sana na mizani ya nguvu kati ya madola inabadilika.

Historia ya Lebanon imejaa mifano inayothibitisha kuwa kutegemea mataifa ya nje, hata kama jambo hilo linaweza kuonekana kuwa na manufaa katika kipindi fulani cha kisiasa, hatimaye hugeuka kuwa gharama ambayo wananchi wa Lebanon hulazimika kuilipa kupitia usalama wao, utulivu, mamlaka ya kitaifa na mustakabali wao.”

Mwisho, alisisitiza kuwa; uhuru wa kweli utakamilika pale wananchi wa nchi hiyo watakapohisi kuwa wako salama, wanaishi katika utulivu na wanaheshimiwa, na pale maamuzi ya Serikali yatakapokuwa yakitokana na maslahi ya Lebanon na wananchi wake, badala ya kuongozwa na hesabu na maslahi ya mataifa ya nje.

Aidha, alirejelea msimamo wa Kamanda wa Jeshi la Lebanon, Jenerali Haikal, aliyesema: “Uhuru haukamiliki isipokuwa kwa kukombolewa ardhi na kupanuliwa mamlaka ya Serikali katika maeneo yote ya nchi.”

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha